1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya uchafuzi wa plastiki yapiga hatua

30 Aprili 2024

Awamu ya nne na ya mwisho ya mazungumzo yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa ya kutafutia ufumbuzi suala la uchafuzi wa mazingira kwa plastiki duniani yalikamilika mjini Ottawa.

https://p.dw.com/p/4fLXR
Mkataba Mpya wa Kimataifa wa Plastiki wa UNESCO
Mtazamo wa jumla wa chumba cha kikao wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha mazungumzo kuhusu mkataba wa kukabiliana na uchafuzi wa plastiki.Picha: Stephanie Lecocq/REUTERS

Kwa mara ya kwanza katika mazungumzo hayo, wajumbe kutoka nchi 175 na waangalizi walijadili rasimu ya kile kitakachokuwa mkataba wa kimataifa wa kukomesha janga la plastiki ambayo hupatikana kila mahali kuanzia vilele vya milima hadi vilindi vya bahari, ndani ya damu na maziwa ya binaadamu.

Soma pia: Viongozi wajadili mkataba wa taka za plastiki

Kikao cha Ottawa kiliendelea kilipoachia katika mazungumzo yake nchini Kenya miezi mitano iliyopita. Aidha wajumbe walikubaliana mfululizo wa mashauriano kati ya sasa hadi Novemba, wakati duru ya mwisho ya mazungumzo itafanyika Korea Kusini.

Mbunge wa Toronto-Danforth nchini Kanada Julie Dabrusin amesema mazungumzo ya Ottawa yamefanikisha kile alichoikiita "mabadiliko makubwa, katika sauti na nishati" ikilinganishwa na duru iliyopita.

"Kwa maelewano, Kanada inaunga mkono pendekezo la mwenyekiti ambalo ni muhimu sana kuendeleza lengo letu kuelekea katika mkutano wa tano wa Kamati ya Majadiliano baina ya Serikali, na tunawasihi wanachama waonyeshe ushirikiano sawa ili kuhakikisha kuwa uamuzi wa mkutano unakubaliwa kwa mara ya kwanza hapa Ottawa ili kujiekea malengo ya mafanikio tutakapofika huko Busan."

Aidha mbunge huyo ameongeza kusema ana matumaini kwamba wanaweza kufikia makubaliano mwisho wa mwaka ili kumaliza uchafuzi kupitia plastiki ifikapo 2040.

Msuguano uliopo?

Uchafuzi wa Plastiki ya Kedonganan Beach nchini Indonesia
Mwanamume akikusanya takataka za plastiki kwenye ufuo uliochafuliwa wakati wa msimu wa mvua za masika katika Pwani ya Kedonganan, nchini Indonesia.Picha: Johannes Panji Christo/picture alliance

Hata hivyo, suala la vizuizi juu ya uzalishaji wa plastiki halikujumuishwa kwenye maandishi ya rasimu hiyo na inasalia kuwa muhimu. Ingawa kuna maafikiano mapana juu ya haja ya mkataba, wanaharakati wa mazingira wanaoomba kupunguzwa kwa uzalishaji wa plastiki wanasalia katika msuguano na mataifa yanayozalisha mafuta na sekta ya plastiki.

Ana Rocha, akizungumza kwa niaba ya eneo la kusini mwa dunia, amesema kumekuwa na nia inayokua ya kushughulikia kemikali za kutengeza plastiki chini ya mkataba huo.

Soma piaUmoja wa Mataifa wajadili uchafuzi wa takataka za plastiki

Peru na Rwanda zilipendekeza katika hoja zao huko Ottawa kupunguza uzalishaji wa plastiki kwa asilimia 40 katika miaka 15 ijayo,  kuendana na malengo ya mkataba wa hewa wa Paris. Walitaja uzalishaji wa plastiki kama kichocheo kikubwa cha ongezeko la joto duniani kwa sababu plastiki nyingi hutengenezwa kutokana na nishati ya kisukuku. Hata hivyo hoja hiyo ilishindwa.

Uzalishaji wa plastiki kwa mwaka umeongezeka zaidi ya mara mbili katika miaka 20 hadi tani milioni 460 na una athari ya kuzidi kuongezeka mara tatu ndani ya miongo minne ikiwa hautadhibitiwa.

 

//AFP, AP