1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiIran

Sheria ya kuvaa hijab kupitiwa upya nchini Iran

29 Aprili 2024

Tume ya Bunge la Iran imeupeleka kwa Baraza la Uongozi lenye ushawishi mkubwa,muswada uliofanyiwa marekebisho kuhusu vazi la hijab ili ufanyiwe tathmini.

https://p.dw.com/p/4fJVY
Iran | Hijab
Vazi la Hijab limekuwa chanzo cha mivutano kati ya wahafidhina na waliberali nchini Iran.Picha: Atta Kenare/AFP/Getty Images

Kulingana na taarifa iliyotolewa na shirika la Tasnim, iwapo muswaada huo wa sheria utaidhinishwa, adhabu kali zinaweza kutolewa kwa wanaokiuka kanuni za mavazi ya taifa hilo la Kiislam, pamoja na kuwataka wanawake kufunika nywele zao hadharani.

Mjadala mkali kuhusu sheria inayopendekezwa umekuwa ukiendelea nchini Iran tangu mwaka jana, huku baadhi ya wabunge wenye misimamo mikali wakisisitiza kwamba adhabu zilizopo ni nyepesi huku wanasiasa wa wastani wakipinga vikali adhabu hizo.

Pendekezo hilo linatoa adhabu kali, ikiwamo kifungo cha hadi miaka 15 jela na kutozwa faini ambayo ni sawa na zaidi ya dola 5,000.

Wanawake wa kigeni wanaweza kufukuzwa nchini humo, na watu mashuhuri kuadhibiwa vikali, rasimu hiyo pia itaweka marufuku ya kitaaluma ya hadi miaka 15.